UJUMBE: KUNA NGUVU KATIKA NENO LA MUNGU
LUKA 5: 4 -11
Tarehe 14.05.2017
Luka aliandika habari zake baada ya kufanya utafiti wa jambo analotaka kuliandikia kama taaluma yake ya utabibu ambapo inamtaka kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kutoa tiba kwa mgonjwa. Luka aliandika habari za Yesu na Simoni Petro kuhusu kushusha nyavu hadi kilindini ili wakavue samaki. Maandiko yanatuambia kuwa wakati Yesu anakutana na akina Simoni Petro muda wa kuvua samaki ulikuwa umepita na walikwisha kuosha nyavu zao ili warudi nyumbani kwani kwa kazi ya usiku ule haikuwa na mafanikio kwa kuwa hawakupata samaki. Ndipo Yesu akawaambia shusheni nyavu zenu mpaka kilindini mkavue samaki. Simoni Petro akajibu Bwana tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha tusipate kitu lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi wakaenda mpaka kilindini wakashusha nyavu zao mara nyavu zao zikaanza kuzama kwa wingi wa samaki wakaamua kuwaita washirika wenzao ili wasaidiane kuchukua samaki. Wakapata samaki wengi sana.
Hebu tuone nguvu ya kuliamini Neno la Mungu
Simoni Petro aliposema kwa Neno lako nitazishusha nyavu kwani alitambua kuwa kazi yao ya usiku kucha haikuwa na mafanikio na wao mahitaji yao yalikuwa ni kupata kitoeo na matumizi mengi kwa familia. Walichoka sana kwa kazi hiyo ya usiku kucha lakini wakaamua kulitii Neno la Mungu na kulitendea kazi kwa kushusha nyavu kama Bwana alivyosema. Je mimi na wewe leo tunaweza kufanya hivyo. Mbona ujumbe unapokuja kwako unaona si wako ila wa mtu mwingine? Hatupokei kutoka kwa Bwana kwa kutoliamini Neno la Mungu.
Ipo nguvu katika kuliamini Neno la Mungu. Neno la Mungu huleta matokeo chanya katika maisha ya mwamini ukiliamini sawa sawa na Neno lake.
Mhubiri
Mchungaji Kiongozi: P. Mneo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni